MATUKIO ya ukatili dhidi ya watoto, bado yameendelea kushika kasi 
kwenye maeneo mbalimbali nchini ambapo katika Mkoa wa Simiyu, mtoto 
mwenye umri wa miaka 17 (jina tunalihifadhi), mkazi wa Bariadi Mjini na 
mwanafunzi wa Shule ya Msingi Bariadi, amejikuta akifungwa minyororo 
mikononi na miguuni kwa miezi minne nyumbani kwa mganga wa kienyeji.
Mganga huyo amefahamika kwa jina la Mdeli Msanja ambaye aliamua 
kufanya ukatili huo baada ya wazazi wa mtoto huyo ambaye anamatatizo ya 
akili, kushindwa kumlipa pesa za matibabu.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Charles 
Mkumbo, alisema wazazi wa mtoto huyo walikubaliana na mganga huyo 
kumlipa sh. 260,000 kama mtoto wao atapatiwa matibabu na kupona.
“Pamoja na wazazi kukubaliana
 na mganga husika, hali ya mtoto haikuweza kubadilika wala kupata unafuu
 hivyo waliomba kumchukua mtoto wao kitendo ambacho kilipingwa na mganga
 kwa madai ya kutolipwa pesa zake ambazo walikubaliana,” alisema.
Alisema mganga huyo aliamua kumchukua mtoto huyo na kumfungia 
chumbani kwake kwa minyororo miguuni na mikononi kwa kipindi cha miezi 
minne akidai pesa zake na kuwapa wakati mgumu wazazi wake.
Kutokana na msimamo wa mganga huyo, mama mzazi wa mtoto huyo Malita James (46), alilazimika kwenda kutoa taarifa Kituo cha Polisi Bariadi kuhusu mateso anayoyapata mwanaye kwa mganga.
“Polisi walishirikiana na 
Dawati la Jinsia kufanya uchunguzi wa tukio hili na walipofika kwa 
mganga, walimkuta akiwa amemfunga minyororo miguuni na mikononi,” alisema Kamanda Mkumbo.
Aliongeza kuwa, polisi walimkamata mganga huyo ambaye hakuwa na kibali cha kutoa tiba za asili, pia alikamatwa na nyara za Serikali ambazo ni pembe moja ya swala na mikia miwili ya nyumbu ambapo uchunguzi ukikamilika atafikishwa mahakamani.
 

 
 
No comments:
Post a Comment