KATIBA MPYA ITAWAENGUA WABUNGE WA ....................
BAADHI ya wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wanakabiliwa na hatari ya kukosa sifa ya kuwania ubunge mwaka 2015, iwapo Bunge Maalumu la Katiba litaridhia pendekezo lililopo katika rasimu
ya sasa, linaloweka sharti la mgombea kuwa na elimu isiyopungua kidato cha nne. Sharti hilo limetajwa katika Rasimu ya Pili ya Katiba iliyowasilishwa hivi karibuni na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu, Joseph Warioba kwa Rais Jakaya Kikwete. Sehemu ya Pili, Ibara ya 125 (1) (b) ya rasimu hiyo, inaweka sharti kuwa mtu yeyote atakuwa na sifa za kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa mbunge endapo anajua kusoma na kuandika Kiswahili au Kiingereza na ana elimu isiyopungua kidato cha nne.Kwa maana hiyo, wabunge wa sasa ambao elimu yao ni chini ya kidato cha nne, hawataruhusiwa kugombea kipindi kingine katika uchaguzi mkuu ujao.Pendekezo hilo ni tofauti kabisa na Katiba ya sasa, ambayo inatambua sifa ya kuwa mbunge ni kujua kusoma na kuandika Kiswahili au Kiingereza.Sehemu ya pili ya Katiba ya sasa, Ibara ya 67 (1) (a), inataja sifa ya kuwa mbunge kuwa ni raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliyetimiza umri wa miaka 21 na ambaye anajua kusoma na kuandika Kiswahili au Kiingereza.Kutokana na sharti hilo la Rasimu ya Pili, kipengele hicho cha elimu kinaweza kuzua mjadala mzito katika Bunge Maalumu la Katiba na baadaye kura ya maoni, kutokana na ukweli kwamba baadhi ya wabunge katika Bunge la Muungano na Baraza la Wawakilishi ambao wote wataingia katika Bunge hilo, wana elimu chini ya kidato cha nne.Orodha hiyo ya wabunge wasio na elimu ya kidato cha nne, ni kutoka vyama vyote vya siasa yaani Chama Cha Mapinduzi (CCM), pamoja na wapinzani jambo linaloweza kuzua mjadala na mvutano wa aina yake katika Bunge hilo.Baadhi ya wananchi na hata wabunge ambao wana elimu ya darasa la saba, wanahoji maana ya Katiba hiyo kuweka kifungu cha kibaguzi kwa baadhi ya Watanzania.Mmoja wa wabunge hao anayetokea moja ya majimbo ya Kanda ya Kati (jina tunalo), aliwahi kuliambia MTANZANIA Jumatatu kuwa kifungu hicho ni cha hatari kwa usalama wa nchi.Alisema kama Katiba inatoa uhuru na haki kwa kila Mtanzania kupiga kura, iweje kupigiwa kura liwe ni kosa kisheria na kikatiba. Alisema anasubiri rasimu hiyo katika Bunge la Katiba, kwa ajili ya kushawishi umma ukatae ubaguzi huo unaoweza kuhatarisha amani na usalama wa nchi kwa sababu Watanzania walio wengi wana elimu ya darasa la saba.
No comments:
Post a Comment