SUGU amkaanga Zitto bungeni
Baada
 ya hapo, kati ya tarehe 14 Januari na 7 Februari, 2013, akaunti ya Leka
 Dutigite Ltd. iliingiziwa jumla ya shilingi 28,600,000. Fedha hizi zote
 ziliingizwa kama fedha taslimu na mtu aitwaye Mchange (shilingi 
3,600,000 tarehe 14 Januari, 2013) na Leka Dutigite (shilingi 25,000,000
 tarehe 23 Januari na 7 Februari, 2013). Kufikia tarehe 7 Februari, 
2013, fedha hizo zote zilikwishatolewa benki.  
Mheshimiwa Spika, Tarehe 28 Februari, 2013, akaunti ya Leka Dutigite
 Ltd. iliingiziwa shilingi 32,367,000 na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya 
Jamii (NSSF). Kwa mujibu wa taarifa za kibenki, siku hiyo hiyo, fedha 
hizo zilitolewa kwenye akaunti hiyo. Siku nne baadae, yaani tarehe 4 
Machi, 2013, NSSF ilifanya malipo mengine kwenye akaunti ya Leka 
Dutigite Ltd., kwa mikupuo miwili, ya jumla ya shilingi 46,663,000. Siku
 hiyo hiyo, fedha hizo nazo zilitolewa kutoka kwenye akaunti hiyo kwa 
mikupuo miwili. Kwa hiyo, katika kipindi cha miezi mitatu katika ya 
tarehe 10 Desemba, 2012 na 4 Machi, 2013, Leka Dutigite Ltd. ililipwa 
shilingi 119,930,000 kwa utaratibu huo huo wa ingiza na toa fasta. Kati 
ya fedha hizo, shilingi 12,200,000 zililipwa na TANAPA na shilingi 
79,027,000 zililipwa na NSSF.  
Hata
 hivyo, Mheshimiwa Spika, mazingira ya malipo haya sio ya kawaida. Hii 
ni kwa sababu ya uwepo wa kampuni ya Gombe Advisors Ltd. Kwa mujibu wa 
nyaraka za BRELA, kampuni hii ilisajiliwa tarehe 24 Novemba, 2011. Kwa 
mujibu wa nyaraka hizo, ofisi za Gombe Advisors Ltd. ziko kwenye jengo 
la City House, Mtaa wa Mkwepu, Dar es Salaam, ziliko ofisi za Leka 
Dutigite Ltd. Kwa mujibu wa nyaraka hizo, wakurugenzi wa Gombe Advisors 
Ltd. ni Zitto Zuberi Kabwe ambaye kazi yake inatajwa kuwa ‘mchumi’, na 
Raphael Ongangi ambaye anatajwa kuwa ‘mchambuzi wa fedha na vitega 
uchumi’ (Financial and Investment Analyst). Bwana Ongangi aliwahi 
kutajwa na gazeti la kila wiki la —– la tarehe 26 Desemba 2013 kuwa ni 
mmoja wa washauri wa Zitto Zuberi Kabwe na anasemekana kuwa msaidizi 
wake.  
Mheshimiwa Spika, Zitto Zuberi Kabwe sio ‘mchumi’ anayetajwa katika 
nyaraka za BRELA zinazoihusu kampuni ya Gombe Advisors Ltd. pekee, bali 
pia ni Mbunge, tangu mwaka 2005, wa Bunge lako tukufu. Kama Mbunge, 
Mheshimiwa Zitto Kabwe ni ‘kiongozi wa umma’ kwa mujibu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, 1995. Sheria hii inawalazimu viongozi wa umma, wanapokuwa madarakani, kuwa “waadilifu,
 wenye huruma, utulivu, umakini na watakaoendeleza viwango vya juu vya 
maadili ili kujenga na kuendeleza imani ya umma kwa uadilifu wa 
Serikali.” 
 
 
 
          
      
 
  
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
No comments:
Post a Comment