Simplfy language

thanx

Thursday, April 3, 2014

Mwaka wa 20 wa kukumbukwa mauaji ya kimbari



Mwezi huu wa Aprili unasadifiana na makumbusho ya mwaka wa 20 wa mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi wa Rwanda. Katika kipindi cha siku 100 kati ya miezi ya Aprili na Julai mwaka 1994, Wahutu wenye misimamo mikali waliua na kuwachinja bila huruma Watutsi waliowachache wapatao laki nane. Wahutu wenye misimamo ya wastani ya kisiasa pia hawakuhurumiwa kwenye mauaji hayo ya umati. Licha ya kuwa wataalamu wa mambo walikuwa tayari wameionya jamii ya kimataifa kuhusiana na uwezekano wa kutokea mauaji hayo, lakini Umoja wa Mataifa haukuchukua hatua yoyote ya maana kwa ajili ya kuyazuia.
Ukweli wa mambo ni kuwa, Wahutu na Watutsi walikuwa wakiishi pamoja kwa amani kwa miaka mingi bila ya kuwepo mivutano mikubwa ya kisiasa wala kijamii. Lakini mara tu baada ya kuingia nchini Rwanda wakoloni wa Ubelgiji na Ufaransa, mbegu za ubaguzi na chuki zilipandwa kati ya makabila hayo mawili. Hivi sasa baada ya kupita miaka ishirini tokea mauaji hayo ya umati yafanyike serikali ya Kigali imeanzisha mradi muhimu wa kukusanya nyaraka na kufanya utafiti wa kina kuhusiana na chanzo cha kutokea mauaji hayo, ili kuzuia kukaririwa tena mkasa kama huo katika siku zijazo. Mwaka 2004 Mahakama ya Kimataifa ya Jinai za Rwanda iliasisiwa mjini Arusha Tanzania ili kuwahukumu wahalifu waliotoa amri ya mauji ya umati dhidi ya Watutsi wa Rwanda, lakini kwa masikitiko makubwa ni faili 60 tu za wahalifu hao ndizo zimeshughulikiwa hadi sasa.
Kwa muda wa miaka 10 iliyopita, mahakama za jadi za Rwanda zinazojulikana kwa jina la Gacaca zimefanya vizuri zaidi kwa kuhukumu na kusuluhisha watu milioni 2 waliohusika na mauaji hayo kwa njia moja au nyingine. Pamoja na hayo, lakini baadhi ya wanaharakati wa haki za binadamu wanazikosoa mahakama hizo kwa kudai kwamba mahakimu wake hawana uzoefu wa kutosha kuhusiana na masuala ya sheria. Wakati huohuo, watetezi hao wa haki za binadamu wana wasiwasi mkubwa wa kupotea nyaraka na vithibitisho vya mauaji ya umati wa Rwanda, kadiri muda unavyozidi kusonga mbele. Hata hivyo maafisa wa Rwanda wanaosimamia vituo vya takwimu na utafiti wanasisitiza kuwa wasiwasi huo haupasi kuwepo kwa sababu nyaraka na vithibitisho hivyo vya kihistoria vinahifadhi vizuri katika vituo vya kisheria nchini. Kujengwa minara ya ukumbusho kwa ajili ya wahanga wa mauaji hayo katika pembe tofauti za nchi pia kunafanyika kwa lengo hilohilo. Kuhusiana na suala hilo, mabaki ya viwiliwili vya wahanga laki mbili na nusu wa mauaji hayo yamewekwa katika jengo la makumbusho ya mauaji hayo lililoko mji mkuu, Kigali.
Katika hali ambayo habari za kutiwa mbarano wahusika wakuu wa mauaji hayo zimekuwa zikisikika katika siku za hivi karibuni katika pembe mbalimbali za dunia, lakini kwa ujumla wananchi wa Rwanda wameamua kufanya juhudi za kusahau mauaji hayo na kuishi pamoja kwa amani na watu waliotekeleza mauaji hayo ya umati, baada ya wao kukiri makosa yao na kuomba msamaha kupitia mahakama za Gacaca. Lililo muhimu hapa ni kujaribu kuzuia kutokea kwa mauaji mengine ya kutisha kama yale yaliyoshuhudiwa nchini humo mwaka 1994.

No comments:

Post a Comment